Omanhene ni chifu wa kijiji. Omanhene mmoja alikuwa na wana watatu, waliokuwa na hamu kubwa ya kuona ulimwengu. Wakaenda kwa baba yao na kuomba ruhusa ya kusafiri. Akawapa ruhusa hiyo bila kusita.
Ilikuwa zamu ya mkubwa kwenda kwanza. Akapewa mtumishi na kila kitu ambacho angeweza kuhitaji kwa safari.
Baada ya kusafiri kwa muda akafika mji mmoja alimoishi Omanhene aliyependa vitendawili. Akiwa mgeni, msafiri, kwa mujibu wa desturi, aliletwa na watu mbele ya chifu.
Chifu akamweleza kwamba walikuwa na sheria fulani kijijini mwao. Sheria moja ilikuwa kwamba kila mgeni lazima amshinde Omanhene katika kujibu vitendawili la sivyo angekatwa kichwa. Lazima awe tayari kuanza shindano asubuhi iliyofuata.
Siku iliyofuata akafika Mahali pa Baraza, na akamkuta Omanhene pale pamoja na watumishi wake wote. Omanhene akauliza vitendawili vingi. Kwa kuwa kijana hakuweza kujibu hata kimoja, akahukumiwa kuwa ameshindwa na akakatwa kichwa.
Baada ya muda mwana wa pili wa Omanhene akaanza safari zake. Kwa bahati ya ajabu akafika mji uleule alimokufa kaka yake. Naye pia akaulizwa vitendawili vingi, na akashindwa kuvijibu. Kwa hiyo naye pia akauawa.
Baada ya muda kaka wa tatu akatangaza nia yake ya kusafiri. Mama yake akafanya kila awezalo kumshawishi abaki nyumbani. Ikawa bure kabisa.
Alikuwa na hakika kwamba naye akifika mji walimokufa kaka zake, jambo lilelile lingemtokea. Badala ya kuruhusu hilo, aliona afadhali afe njiani.
Akamwandalia chakula kiitwacho kenkey ambacho alikijaza sumu. Baada ya kukipakia ndani ya mfuko wake, akaanza safari. Punde akaanza kuhisi njaa. Hata hivyo, akijua kwamba mama yake hakutaka aondoke nyumbani, na kwa hiyo huenda ameweka sumu katika chakula, akaona akijaribu kabla ya kula yeye mwenyewe. Alipomwona tumbusi karibu, akamtupia nusu ya mkate.
Ndege akala kenkey, na mara moja akaanguka akafa kando ya njia. Chui watatu wakapita na kuanza kumla tumbusi. Nao pia wakaanguka wakafa.
Kijana akakata sehemu ya nyama ya chui na kuichoma. Kisha akaipakia kwa uangalifu ndani ya furushi lake.
Mbele kidogo akashambuliwa na wanyang'anyi saba wa barabarani. Walitaka kumuua mara moja. Akawaambia alikuwa na nyama nzuri iliyochomwa ndani ya furushi lake na akawakaribisha kwanza wale pamoja naye. Wakakubali na kugawa chakula mafungu manane.
Walipokuwa wakila kijana akaficha fungu lake kwa uangalifu. Punde wanyang'anyi wote saba wakaugua na kufa. Kisha kijana akaendelea na safari yake.
Mwishowe akafika mji walimokufa kaka zake. Kama wao, aliitwa Mahali pa Baraza kujibu vitendawili vya Omanhene. Kwa siku mbili shindano likawa sare. Mwishoni mwa muda huo, kijana akasema, "Nimebakiwa na kitendawili kimoja tu. Ukiweza kukijibu, unaweza kuniua." Kisha akampa Omanhene kitendawili hiki:
Nusu inaua mmoja
Mmoja anaua watatu
Watatu wanaua saba.
Mtawala akashindwa kukijibu jioni ile, kwa hiyo kikaahirishwa hadi siku iliyofuata.
Usiku Omanhene akajibadilisha sura na kwenda kwenye nyumba alimokaa mgeni. Pale akamkuta kijana amelala ukumbini.
Akidhani mtu aliye mbele yake ni mtumishi wa mgeni, na bila kuota hata kidogo kwamba ni mgeni mwenyewe, akamwamsha aliyelala na kumwahidi zawadi kubwa kama angempa jibu la kitendawili.
Kijana akajibu kwamba angemwambia jibu kama Omanhene angemletea vazi ambalo daima alivaa Barazani.
Mtawala alifurahi sana kwenda kumletea. Kijana alipokuwa ameyashika mavazi salama kabisa, akamweleza Omanhene mjanja kitendawili kikamilifu. Akasema kwamba walipokuwa wakiondoka nyumbani, mama wa bwana wake alimwandalia kenkey. Ili kujua kama kenkey ni salama, walimpa tumbusi nusu yake. Tumbusi akafa. Chui watatu walioonja tumbusi nao wakafa. Nyama kidogo iliyochomwa ya chui ikawaua wanyang'anyi saba.
Omanhene alifurahi sana kugundua jibu. Akamwonya yule aliyedhaniwa kuwa mtumishi asimwambie bwana wake kilichotokea.
Asubuhi wanakijiji wote wakakusanyika pamoja tena. Omanhene kwa fahari akatoa jibu la kitendawili kana kwamba yeye mwenyewe alikuwa amelibaini. Lakini kijana akamwomba alete vazi lake la sherehe, ambalo alipaswa kuwa amelivaa Barazani. Bila shaka, hakuweza kufanya hivyo, kwa kuwa kijana alikuwa amelificha kwa uangalifu.
Kisha mgeni akaeleza kilichotokea usiku, na jinsi mtawala alivyopata jibu la kitendawili kwa udanganyifu.
Baraza likatangaza kwamba Omanhene ameshindwa kujua kitendawili na lazima afe. Kwa hiyo akakatwa kichwa na kijana akateuliwa kuwa Omanhene mahali pake.
