Wakati mmoja chui hawakujua jinsi ya kukamata wanyama ili wapate chakula. Akijua kwamba paka alikuwa hodari sana katika jambo hili, siku moja Chui alikwenda kwa Paka na akamwomba kwa adabu sana amfundishe ufundi huo. Paka akakubali bila kusita.
Jambo la kwanza Chui alilopaswa kujifunza lilikuwa kujificha vichakani kando ya njia, ili asionekane na mnyama yeyote anayepita. Kisha, alipaswa kujifunza jinsi ya kutembea msituni bila kelele. Kamwe asimruhusu mnyama anayemfukuza ajue kwamba anamfuata. Kanuni kuu ya tatu ilikuwa jinsi ya kutumia makucha na upande wake wa kushoto kumrukia mawindo yake.
Baada ya kumfundisha mambo haya matatu, Paka akamwomba aende akayazoeze vizuri. Akishayajua kikamilifu angeweza kurudi kwake naye angempa masomo zaidi ya uwindaji.
Chui akatii. Mwanzoni alifanikiwa sana na akapata chakula chote alichotaka. Hata hivyo, siku moja hakuweza kukamata chochote kabisa.
Akiwa na njaa kali, akawaza angekula nini jioni hiyo. Ghafla akakumbuka kwamba paka alikuwa na familia kubwa. Akaenda moja kwa moja nyumbani kwake na akakuta hayupo.
Bila kufikiria hata kidogo wema aliotendewa, Chui alikumbuka tu kwamba alikuwa na njaa, akawala watoto wote wa paka. Paka alipogundua jambo hili la kutisha, alikasirika mno hadi akakataa kuwa na uhusiano wowote tena na kiumbe huyo mkubwa.
Kwa hiyo chui hajawahi kuweza kujifunza jinsi ya kukamata wanyama wanaompita upande wake wa kulia.
