Kwofi alikuwa mwana mkubwa wa mkulima aliyekuwa na wake wawili. Mama yake Kwofi hakuwa na watoto wengine.
Mvulana alipokuwa na umri wa miaka mitatu mama yake alifariki. Kwofi akakabidhiwa kwa mama yake wa kambo amlee. Baada ya hapo mama huyo akazaa watoto wengi. Bila shaka, Kwofi ndiye aliyekuwa mkubwa kuliko wote.
Alipokuwa na umri wa miaka kumi hivi baba yake naye akafariki. Sasa Kwofi hakuwa na ndugu yeyote isipokuwa mama yake wa kambo, ambaye alilazimika kumfanyia kazi.
Alipokuwa akikua, mama wa kambo aliona jinsi alivyokuwa mwerevu zaidi na mzuri zaidi kuliko watoto wake mwenyewe, na akaanza kumwonea wivu mkubwa. Alikuwa mwindaji hodari kiasi kwamba siku baada ya siku alirudi nyumbani akiwa amebeba nyama au samaki.
Kila siku alimtendea kwa namna ileile. Alipika nyama, kisha akaigawa. Alimpa kila mmoja fungu kubwa, lakini ilipofika zamu ya Kwofi alikuwa akisema, “Ah, mwanangu Kwofi, hakuna iliyobaki kwa ajili yako! Lazima uende shambani ukachume papai lililoiva.” Kwofi hakuwahi kulalamika. Hata mara moja hakuwahi kuonja nyama aliyoiwinda. Katika kila mlo wengine walipewa, lakini haikutosha kamwe kwa ajili yake.
Jioni moja, jambo la kawaida lilipokuwa limetokea, Kwofi alikuwa akijiandaa kwenda shambani kuchukua papai kwa ajili ya chakula chake cha jioni. Ghafla mmoja wa miungu akatokea kijijini, akiwa amebeba mfuko mkubwa begani. Akawaita wanakijiji wote pamoja kwa maneno haya: “Enyi wanakijiji wangu, nimekuja na mfuko wa kifo kwa ajili yenu!”
Hapo akaanza kugawa vilivyokuwa ndani ya mfuko wake miongoni mwao. Alipomfikia Kwofi akasema: “Ah, mwanangu Kwofi, nyama haikuwahi kukutosha, wala hakuna kifo kwa ajili yako.”
Aliposema maneno haya kila mtu kijijini akafa isipokuwa Kwofi. Akaachwa atawale pale kwa amani, na akafanya hivyo kwa furaha kubwa.
