Karne nyingi zilizopita, watu wa dunia hii walisumbuliwa sana na mafuriko. Mara kwa mara bahari ilikuwa ikivuka mipaka yake ya kawaida na kufurika juu ya maeneo ya chini yenye mchanga yaliyopakana nayo. Jambo hili lilitokea tena na tena, na maisha mengi yalipotea katika kila mafuriko. Binadamu walihangaika sana kutafuta njia ya kuepuka maafa haya yaliyojirudia mara kwa mara. Hawakuweza kubuni njia yoyote ya kuyaepuka.
Kwa bahati nzuri kasa mwenye hekima akaja kuwasaidia. “Fuateni ushauri wangu,” akasema, “mpande safu za minazi kando ya pwani. Itaushikilia mchanga pamoja na kuuzuia usisombwe kwa urahisi.” Wakafanya hivyo, na wakafanikiwa sana. Mizizi ya minazi iliushikilia mchanga imara mahali pake. Wakati ulipofika tena wa bahari kufurika, maji yalifika tu hadi kwenye mstari wa miti na hayakwenda mbele zaidi. Hivyo maisha mengi yaliokolewa kila mwaka kwa busara ya kasa mwema.
Kwa kulipa wema huo, mtu angedhani binadamu wangemlinda na kumthamini mnyama huyu maskini. Lakini hapana! Kila mara kasa anapokuja ufukweni kutaga mayai yake mchangani, anakamatwa na kuuawa kwa ajili ya nyama yake. Ni wazo la utovu wa shukrani wa binadamu kwake ndilo linalomfanya ajipige kifua kwa miguu yake ya mbele anapokamatwa. Anaonekana kana kwamba anasema, “Ah! Hili ndilo tu ninalolipwa kwa wema wangu kwenu.”
.png?ngsw-bypass=1)