Dunia nzima ilikuwa imejaa maji Mungu alipoamua kuumba ulimwengu. Mungu akamtuma mjumbe wake Obatala kufanya kazi ya kuumba ulimwengu. Obatala akaenda na msaidizi wake, mtu aitwaye Oduduwa, pamoja na kibuyu kilichojaa udongo na kuku. Kisha wakaanza kushuka duniani kwa kamba.
Njiani, wakasimama kwenye karamu ambapo Obatala akalewa kwa kunywa mvinyo wa mnazi kupita kiasi. Oduduwa, alipomkuta bwana wake amelewa, akachukua kibuyu na kuku na akaendelea na safari.
Oduduwa alipofika duniani, akanyunyiza udongo kutoka kwenye kibuyu juu ya maji na akamwachia kuku juu ya udongo. Kisha kuku akakimbia huku na huko akitawanya udongo kila upande alioelekea hadi kukawa na nchi kavu. Oduduwa alikuwa ameumba ardhi kutokana na kile kilichokuwa maji.
Baadaye Obatala alipozinduka kutoka kwenye ulevi wake, aligundua kwamba Oduduwa alikuwa ameshaifanya kazi yake, naye akakasirika sana. Hata hivyo, Mungu akampa kazi nyingine ya kufanya: kuwaumba watu ambao wangeijaza dunia.
Na hivyo ndivyo ulimwengu ulivyoumbwa mahali ambapo sasa panaitwa lle-Ife.
