Hapo zamani za kale, wanyama wote waliishi pamoja kwa umoja. Walikula chochote walichoweza kupata pamoja. Hali hii iliendelea kwa muda mrefu sana hadi jambo fulani lilipotokea lililosababisha vurugu kubwa miongoni mwa wanyama.
Kilichotokea ni kwamba kulikuwa na njaa kubwa bila chakula wala majani mabichi kwa wanyama kula. Hii ilitokea kwa sababu wanyama walikuwa hawajapata mvua kwa muda mrefu katika eneo lao. Kisha wanyama wakaamua kufanya mkutano juu ya la kufanya ili kujiweka hai pamoja na watoto wao. Katika mkutano huo, wanyama kwa kauli moja waliamua kwamba wangewaua wazee miongoni mwao mmoja mmoja ili wawale pamoja kuzuia njaa. Wanyama wazee walikubaliana na uamuzi huu na wanyama walikuwa wakileta wazee wao kuliwa zamu yao ilipofika. Punde wanyama wengi wazee walikuwa wamekwisha. Baadhi ya wanyama waliamua kutowatoa mama zao kwa uamuzi kama huo. Mbwa alikuwa mmoja wa wanyama hawa. Mbwa alipotambua kwamba zamu yake inakaribia, alimchukua mama yake hadi kwenye mti mkubwa wa mvule, wote wawili wakapanda juu ya mti hadi wakaweza kugusa anga.
Kisha mbwa akampeleka mama yake mbinguni na wote wawili wakala hadi wakashiba, na mbwa akarudi duniani. Aliporudi, mbwa akakutana na rafiki yake kobe aliyemuuliza kuhusu mama yake na mbwa akamwarifu kobe kwamba mama yake amekufa na kwamba kobe aje kuona alipomzika (mbwa alikuwa amechimba kaburi upesi nyuma ya nyumba yao na kulifunika kwa mchanga uliochimbwa karibuni mara tu aliporudi kutoka kumficha mama yake). Kobe alipoona kaburi lililochimbwa karibuni, aliamini kwamba mama wa mbwa alikuwa ndani ya kaburi. Muda mfupi baadaye, wanyama wakamjulisha mbwa amlete mama yake kwamba ilikuwa zamu yake. Mbwa akawaambia kwamba mama yake amekufa, na waje kuona alipozikwa. Kobe akathibitisha hili, na wanyama wakaridhika.
Ikatokea kwamba mbwa alikuwa na njaa na akakimbilia kwenye mti wa mvule na kuanza kuimba “mama, mama nishushie kamba. Wanyama wote wanaua mama zao kwa chakula lakini mimi mbwa nilimficha mama yangu mbinguni; mama shusha kamba”. Mama yake akashusha kamba na mbwa akapanda upesi kufanya karamu na kula pamoja na mama yake. Mara tu alipomaliza kula, mbwa akashuka ameshiba na mwenye furaha. Wanyama wote walionekana wamedumaa na wenye njaa daima. Wanyama walishangaa kwamba mbwa alionekana mnene na mzuri. Wakamuuliza mbwa alikuwa akila nini tofauti na chakula chao kwa sababu alionekana mnene na mwenye afya. Akawaambia kwamba alikuwa akinywa supu ya kokwa za mawese na ndiyo sababu alikuwa mnene sana. Kobe akamwomba rafiki yake ampe supu hiyo. Mbwa akampa, na kobe akashiba sana baada ya kunywa supu. Baada ya muda, kobe akaona njaa sana tena. Kisha kobe akaanza kumshuku mbwa kwamba hakuwa akisema ukweli.
Kobe akaanza kumfuatilia mbwa bila mbwa kujua. Siku moja ya bahati mbaya, mbwa alikwenda kwenye mti wa mvule kama kawaida alipokuwa na njaa na kuanza kuimba: “mama, mama nishushie kamba. Wanyama wote wanaua mama zao kwa chakula lakini mimi mbwa nilimficha mama yangu mbinguni; mama shusha kamba”. Mama yake akashusha kamba na mbwa akapanda upesi kufanya karamu na kula pamoja na mama yake. Mara tu alipomaliza kula, mbwa akashuka ameshiba na mwenye furaha akaenda kulala. Mara tu mbwa alipolala, kobe akatoka mafichoni mwake nyuma ya kichaka na kwenda mahali pa mti wa mvule. Akaanza kuimba: “mama, mama nishushie kamba. Wanyama wote wanaua mama zao kwa chakula lakini mimi mbwa nilimficha mama yangu mbinguni; mama shusha kamba”. Mama wa mbwa akashusha kamba akijiuliza kama mwanawe hakuwa ameshiba. Kobe akapanda polepole mno hivi kwamba mama wa mbwa ikabidi atazame chini kuona kwa nini mwanawe anachelewa hivyo kupanda. Kwa mshangao wake, akaona kwamba ni kobe aliyekuwa akipanda na si mwanawe. Kobe alikuwa karibu robo tatu ya njia kufika juu. Kisha mama wa mbwa akakata kamba na kobe akaporomoka chini mgongo wake ukivunjika vipande vipande. Siafu wakubwa wafanyakazi walikuwa wakipita na kobe akawasihi wamsaidie kuunganisha mgongo wake. Wakakubali na walipomaliza, ngozi ya mgongo haikuwa sawa tena. Ngozi ya mgongo haikuwa laini tena bali ilikuwa na mikwaruzo mingi. Hii ndiyo sababu ngozi ya mgongo wa kobe ina mikwaruzo mingi hadi leo.
.jpeg?ngsw-bypass=1)