Zamani sana watu hawakujua kitu chochote. Hawakujua jinsi ya kupanda mazao, wala jinsi ya kufuma nguo, wala jinsi ya kutengeneza zana za chuma. Mungu Nyame aliyekuwa juu angani alikuwa na hekima yote ya ulimwengu. Aliihifadhi salama ndani ya chungu cha udongo.
Siku moja, Nyame aliamua kwamba angempa Ananse chungu cha hekima. Kila mara Ananse alipotazama ndani ya chungu cha udongo, alijifunza kitu kipya. Ilikuwa ya kusisimua mno!
Ananse mroho akawaza, “Nitakiweka chungu salama juu kabisa ya mti mrefu. Kisha nitaweza kuwa nacho peke yangu!” Akasokota uzi mrefu, akauzungusha kwenye chungu cha udongo, na akaufunga tumboni mwake. Akaanza kupanda mti. Lakini ilikuwa vigumu kupanda mti huku chungu kikimgonga magotini kila wakati.
Muda wote huo mwana mdogo wa Ananse alikuwa amesimama chini ya mti akitazama. Akasema, “Je, haingekuwa rahisi zaidi kupanda kama ungefunga chungu mgongoni badala yake?” Ananse akajaribu kufunga chungu cha udongo kilichojaa hekima mgongoni mwake, na kweli ikawa rahisi zaidi.
Muda si mrefu akafika juu kabisa ya mti. Lakini kisha akasimama na kuwaza, “Mimi ndiye ninayepaswa kuwa na hekima yote, kumbe mwanangu ana akili kuliko mimi!” Ananse akakasirika sana kwa jambo hili hadi akakitupa chungu cha udongo chini kutoka juu ya mti.
Kikavunjika vipande vipande ardhini. Hekima ikawa huru kwa kila mtu kuishiriki. Na hivyo ndivyo watu walivyojifunza kulima, kufuma nguo, kutengeneza zana za chuma, na mambo mengine yote ambayo watu wanajua kuyafanya.