Hapo zamani za kale Kunguru hakuwa na manyoya imara. Alikuwa na manyoya laini tu. Hakuweza kuruka vizuri. Mara nyingi aliona baridi na hakuwa na furaha. Alikosa furaha zaidi mvua ilipokuwa ikinyesha. Aliona baridi.
Kunguru Mweupe alikuwa ndege mwenye furaha zaidi kuliko Kunguru. Alikuwa na manyoya meusi imara mwili mzima. Aliweza kuruka hadi mahali popote alipopenda. Daima alikuwa na joto.
Tai alikuwa mfalme wa ndege wote. Aliishi juu ya mti mrefu kwenye mlima mrefu.
Siku moja Mfalme Tai akamwambia mkewe, “Nataka kuona ni yupi kati ya watu wangu anayevaa vizuri kuliko wote. Nitampa zawadi.”
Wajumbe wa Mfalme Tai wakawaambia ndege wote, “Mkivaa vizuri, mfalme atawapa zawadi.” Kila mtu alitaka manyoya mapya. Kunguru maskini sasa alikosa furaha kuliko wakati wowote. Alitaka kuazima manyoya kutoka kwa ndege wengine. Lakini hakuna aliyempa hata moja.
Mwishowe Kunguru akaenda kwa Kunguru Mweupe. Akasema, “Kunguru Mweupe, tafadhali, niazime manyoya kadhaa. Nataka kuvaa vizuri nipate zawadi ya mfalme. Tafadhali, niazime manyoya yako mazuri. Nitakurudishia.”
Kunguru Mweupe akampa Kunguru manyoya mengi meusi. Kunguru akaweka manyoya mgongoni na mabawani mwake. Alionekana mzuri sana.
Mfalme akatuma wajumbe wake kuwaita ndege wote. Mfalme Tai akaketi juu ya kigoda chake kirefu. Mkewe akaketi karibu naye. Kisha ndege wote wakaja. Kulikuwa na ndege wengi wa aina tofauti.
Mmoja mmoja ndege wakajionyesha kwa mfalme na malkia. Wote walikuwa wazuri, lakini baadhi walikuwa wazuri kuliko wengine. Kunguru alikuwa mzuri kuliko wote.
Malkia akamwambia mfalme kwa upole, “Mimi nampenda Kunguru kuliko wote”
Mfalme Tai akawaambia ndege, “Kunguru ni wa kwanza! Sasa hii ndiyo zawadi yake: atakapokufa hakuna mnyama atakayeula mwili wake.”
Ndege wengine wote wakampigia Kunguru makofi. Kisha wote wakarudi nyumbani.
Kunguru alipofika nyumbani akasema, “Nitamrudishia Kunguru Mweupe manyoya yake kesho.” Kesho ikafika lakini Kunguru hakurudisha manyoya. Miezi mingi ikapita, lakini Kunguru hakurudisha manyoya.
Kisha Kunguru Mweupe akakasirika. Siku moja akaenda nyumbani kwa Kunguru. Kunguru alipomwona Kunguru Mweupe, Kunguru akaanza kukimbia. Kunguru Mweupe akamfukuza na kumkamata. Akachukua baadhi ya manyoya. Kunguru aliendelea kukimbia muda wote. Kisha Kunguru akaruka angani. Kunguru Mweupe akamfuata akaruka na kuchukua manyoya zaidi. Kunguru Mweupe akaanza kulia:
“Nipe manyoya yangu!
Nipe manyoya yangu!”
Hii ndiyo sababu kunguru mweupe mara nyingi huruka na kulia akimfuata kunguru. Lakini hatakula mwili wa kunguru.
