Hii ni hadithi ya Cierume, shujaa anayecheza ngoma kutoka Mbeere aliyewaua wanaume kwa fimbo yake ya ngoma.
Cierume alizaliwa wakati fulani katika karne ya 19, kabla wazungu hawajawahi kukanyaga ardhi ya Mbeere. Jina lake linaweza kusemwa kuwa lilitokana na neno "urume", linalomaanisha ukali au ujasiri. Msichana huyu kweli aliishi kulingana na jina lake.
Kadiri muda ulivyopita msichana Cierume akakua kuwa mwanamke, na tabia yake ikakua pia, na watu wakaigundua upesi.
Siku moja, kulikuwa na matatizo katika ardhi ya Mbeere. Kundi la watu wa kabila la Wakamba, chini ya uongozi wa kiongozi wao wa kutisha na asiye na huruma, waliishambulia nchi, wakipora na kuua, wakitia hofu mioyoni mwa Waembu. Hata wanaume wa Kiembu walikuwa hoi na wameshindwa. Kulikuwa na kukata tamaa nchini. Cierume jasiri akaamua kujiunga na wanaume wa Kiembu kupigana dhidi ya wavamizi. Kweli alikuwa jasiri na anayestahili jina lake.
Kama mwanamke kupigana bega kwa bega na watu wa kabila lake hakukushangazi, labda chaguo lake la silaha litakushangaza. Wakati wanaume walikimbilia vitani wakiwa na mapanga ghafi, panga ndefu na mikuki, Cierume aliingia vitani na fimbo yake. Fimbo ya ngoma ambayo yeye na wanawake wengine waliitumia katika ngoma zao za jadi. Haijulikani kwa hakika kama ni kumwona mwanamke akikimbilia vitani au ukweli kwamba mwanamke huyu alikuwa amebeba fimbo ndiko kulikowashangaza mashujaa wa Kikamba na kuwachanganya hadi wakashindwa. Kushoto na kulia, watu wa kabila la Wakamba walianguka kwa fimbo ya Cierume. Hata kiongozi wa kutisha wa mashujaa wa Kikamba hakuweza kumshinda. Alishindwa kwa aibu. Alipaswa kujua kwamba asingepigana (au kucheza ngoma?) na mwanamke mwenye fimbo na kushindwa. Hivyo ndivyo Cierume alivyopata ngao yake ya kwanza ya vita, zawadi ya ushindi dhidi ya Wakamba.
Habari za matendo yake punde zikawa midomoni mwa kila mtu Mbeere. Inasemekana kwamba huko Mbeere na Embu, hakuna mwanamke aliyeweza kulinganishwa na Cierume. Hata miongoni mwa Wakamba, Wakikuyu na Wameru, ni wanawake wawili tu walioweza kulinganishwa naye. Ciokaraine binti Barungu kutoka Meru na mwanamke wa Kikikuyu aitwaye Wangu.
Muda mfupi baadaye, Cierume aliteuliwa kushika nafasi ya uongozi. Akiwa kiongozi mwanamke pekee katika baraza la Wambeere, Cierume aliwaonewa wivu na baadhi ya wanaume walioona kwamba hakuwa na haki ya kuongoza miongoni mwao. Baadhi ya wanaume hata walifika hatua ya kumsema vibaya, wakieneza uvumi na kuhoji uwezo wake wa kuongoza wakisema mila haziruhusu. Wakati mmoja, mwanamume mmoja alimtukana lakini Cierume hakumjibu neno. Badala yake alisimama mbele yake na kumpiga bila huruma mbele ya wenzake. Alikuwa na bahati kuokolewa na wenzake kutoka kwenye hasira yake. Umaarufu wake uliendelea kukua kiasi kwamba aliteuliwa kuwa chifu wa watu wa Mbeere wakati wa ukoloni.
Alipigania bila hofu haki za watu wake dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Alikuwa jasiri kiasi kwamba inasemekana alimtukana kwa hasira Mkuu wa Wilaya wa Kizungu alipokuwa akilalamikia utumwa wa kulazimishwa kwa watu wake.
Mwishowe, Cierume alipoteza uchifu wake kutokana na njama ya wanaume wenye wivu. Licha ya hayo, urithi wake unaendelea kuishi na jina lake linaendelea kuwahamasisha wanawake wa Embu kuonyesha dhamira katika kila wanalofanya.
