Hapo zamani za kale, aliishi mvulana aliyeitwa Mafani.
Siku moja, Mafani akamjia bibi yake na kusema, "Bibi mpendwa, tafadhali nipe panga! Nataka kwenda kutega mitego ya ndege!"
"Siwezi kukupa panga, mwanangu. Naogopa utajiumiza," bibi yake akajibu.
Lakini Mafani hakukata tamaa kwa urahisi. Akaokota kigae cha chungu cha kupikia, akanoa ncha yake moja juu ya jiwe, na kukitumia badala ya panga. Kisha akaenda kukata vichipukizi kadhaa virefu vyembamba, akavipaka utomvu mzito unaonata aliouandaa kutoka kwa majimaji ya mti wa ulimbo, na kuvipanda katikati ya kipande cha nyasi.
Alikuwa ametega mitego kwa shida tu hua alipotua juu ya mmoja wao na kunaswa. Mafani akampeleka hua kibandani kwake na kumwandaa kwa ajili ya mlo wake wa mchana. Hata hivyo, bibi yake akamchukua ndege na kumla yeye mwenyewe.
Kisha Mafani akamwambia bibi yake, "Nilipokuomba panga, hukutaka kunipa, lakini sasa umekula ndege wangu. Ni haki tu unilipe." Na bibi yake akampa panga.
Mafani akachukua panga na kwenda safarini. Njiani, akakutana na watu waliokuwa wakijenga bwawa ili wawe na maji ya kutosha kwa kiangazi. Walikuwa wakipata shida kugongomea nguzo kwa sababu hazikuwa zimechongwa vizuri.
Mafani akawatazama kwa muda. Mwishowe, akawaendea na kusema, "Kwa nini msichonge nguzo zenu? Ni ujinga ulioje kupoteza muda na nguvu zenu hivi!"
"Lakini hatuna panga la kuchongea nguzo," watu wakajibu.
"Nina panga bora sana hapa, kali kiasi cha kukata gogo," akasema Mafani. "Naweza kuwaazima mkipenda!"
Kwa hiyo wakachukua panga la Mafani na kuchonga nguzo zao. Lakini katika hamu yao ya kumaliza haraka, walilitumia panga kwa ukali kiasi na kulivunja vipande viwili.
Kisha Mafani akasema, "Mmevunja panga langu na lazima mlilipe." Nao wakampa vibuyu kadhaa vilivyojaa maji ya kunywa. Akavichukua na kuendelea na safari yake.
Baada ya muda, akakutana na watu waliokuwa wakikusanya kumbikumbi wa kuliwa. Wakiwa wamekaa juani kwa muda, waliteseka kwa kiu. Mafani alipofika, wakamsihi awape maji kidogo.
"Niko tayari kuwasaidia, lakini msiyanywe yote," akasema Mafani. Lakini watu walipoonja maji, wakaendelea kunywa hadi tone hata moja halikubaki. Mafani akasema, "Sasa nilipeni maji!" Nao wakampa kipimo cha kumbikumbi.
Mafani alipokuwa akipita, akaona ndege wakishughulika kukusanya mbegu za mafuta kwa ajili ya mlo wao wa jioni. Akawakaribia na kusema, "Kwa nini mnakula mbegu hizi? Hakika zitawafanya muugue. Mngejaribu baadhi ya kumbikumbi hawa badala yake. Haya, karibuni mjipakulie, lakini nirudishieni wanaobaki!" Naye akawakabidhi kipimo cha kumbikumbi.
Ndege wakaanza kula na kuendelea kula hadi kumbikumbi wa mwisho akatoweka. Kisha Mafani akawaambia ndege, "Sasa kwa kuwa mmekula kumbikumbi wote, ni haki tu mnilipe." Ndege waliposikia hivi, wakaruka hadi kwenye mti uliokuwa karibu na kuchuma matunda mengi, waliyompa badala ya kumbikumbi. Mafani akachukua matunda na kuendelea.
Baada ya kusafiri umbali fulani, akafika kwenye kilima kikubwa. Alikuwa amechoka mno kupanda kilima akiwa na mzigo kichwani, kwa hiyo akajitupa chini kivulini mwa mnazi kupumzika. Pale akakutana na kundi la wawindaji. Walikuwa na njaa sana na wakayatazama matunda ya Mafani kwa tamaa. Mafani alipoona hivi, akawaambia watu wajipakulie. Kwa muda mfupi, walikuwa wameyala matunda yote, bila kuacha hata kidogo.
Jambo hili halikumpendeza Mafani hata kidogo, naye akasema, "Sikilizeni, rafiki! Niliwakaribisha mjipakulie matunda kidogo, lakini sikuwapa ruhusa kuyala yote. Sasa kwa kuwa mmeyala yote, lazima nisisitize mnilipe." Nao wakamlipa paja la nguruwe.
Mafani alipoendelea, akafika kwenye kibanda cha upweke ambamo bibi kizee alikuwa akikausha chumvi motoni. Akaweka nyama aliyopewa na wawindaji motoni ili ichomwe. Ilipoiva vizuri, bibi kizee akaichukua na kuila yote. Kisha Mafani akamwambia mwanamke, "Kwa kuwa umekula nyama yangu yote, ni haki tu uilipe." Mwanamke akakubali na kumpa kipimo cha chumvi.
Muda mfupi baadaye, Mafani alipokuwa akipita juu ya kilele cha kilima, akakutana na Upepo, uliokuwa ukisukuma mbele yake majani makavu na nyuzi kutoka kwa msufi uliokuwa karibu. "Ni ujinga ulioje," Mafani akaambia Upepo. "Ungechukua chumvi yangu kidogo badala yake." Upepo ukaishika chumvi, na kufumba na kufumbua, yote ikatoweka.
Kisha Mafani akaambia Upepo, "Sikukuambia uchukue sehemu tu ya chumvi yangu? Sasa kwa kuwa umeichukua yote, unapaswa kuilipa." Kisha Upepo ukaita upepo mwingine, ukaunasa ndani ya mfuko, na kumpa Mafani mfuko wa upepo.
Mafani alipoendelea, akakutana na mke wa chifu aliyekuwa akipepeta mahindi. Mafani akamwambia mwanamke, "Ni ajabu ulioje kwamba wewe, mke wa chifu mwenye nguvu, upepete mahindi mwenyewe! Kwa nini usitumie upepo kidogo ulio katika mfuko wangu?"
Mwanamke akachukua mfuko na kuufungua ili atumie upepo. Mara moja, vumbi lote na makapi yakapeperushwa, yakibaki tu mahindi safi yaliyojaa. Lakini mfuko uliokuwa na upepo sasa ulikuwa mtupu. "Kwa nini umetumia upepo wote?" Mafani akauliza. "Sasa lazima uulipe. Nilikuwa tayari kukufanyia hisani, lakini sipendi kudanganywa!" Mwanamke, akiwa na uwezo, akamlipa kipimo maradufu cha mahindi.
Baada ya Mafani kumwacha mwanamke, akaona kundi la njiwa pori kando ya njia, wakishughulika kudonoa matunda madogo. Akawaambia, "Jamani! Mnawezaje kuishi kwa chakula duni namna hii? Kwa nini msijaribu mahindi yangu kidogo?" Naye akafungua mfuko wake na kuuweka mbele yao.
Kwa muda mfupi usioaminika, njiwa walikuwa wameyala mahindi yote. Hata punje moja haikubaki. Mafani alipowataka njiwa walipe mahindi, wakampa kipimo cha mbegu za mafuta. Kutoka kwa hizo akatengeneza mafuta, akayatia ndani ya kibuyu, na kuendelea.
Akafika kwenye mji ambamo mwanamke mmoja alikuwa amefariki. Walikuwa wakifanya maandalizi ya mazishi yake. Kila kitu walichohitaji kilikuwepo isipokuwa kitu kimoja muhimu sana—mafuta ya kupaka mwili. Mafani aliposikia taabu yao, akawapa mafuta yake kidogo. Baada ya kutumia tone la mwisho, Mafani akadai mafuta mengine badala yake. Wakishindwa kulipa, wakampa maiti ya mwanamke. Mafani akachukua maiti na kuondoka.
Alipokaribia mji mwingine, akachukua maiti, akaiegemeza kwenye mti ukingoni mwa genge, na kuingia mjini, ambapo shindano la mieleka lilikuwa likifanyika. Mafani akasimama na kutazama kwa muda. Kisha akamwambia mmoja wa wanawali waliokuwa karibu, ambaye uzuri wake na mavazi yake ya thamani yalikuwa yamemvutia, "Nakuomba, nenda ukamwite mke wangu, anayenisubiri nje kidogo ya mji. Jina lake ni Mawum."
Mwanamwali akaenda na kumkuta mwanamke ameegemea mti, akionekana amelala usingizi mzito. Akaita, "Mawum! Mawum!" Kusipokuwa na jibu, akaenda kumwamsha. Lakini alipougusa mwili, ukaanguka na kubingirika chini ya genge.
Mwanamwali alitishika mno. Alipopona vya kutosha kutokana na mshtuko, akarudi mbio na kumwambia Mafani, "Mke wako ameanguka chini ya genge!" Mafani akamwambia mwanamwali, "Umefanya nini? Nitamwajibisha baba yako kwa hasara yangu!" Kisha baba wa mwanamwali akampa Mafani binti yake na kusema, "Mchukue; ni wako. Na awe uhai wa uhai wako na furaha ya moyo wako."
Mafani akamchukua bibi arusi wake na kurudi kwa bibi yake. Waliishi pamoja kwa furaha sana na wakafikia uzee mwema.
