Hapo zamani za kale, palikuwa na nchi ambayo watu wake walipenda kucheza ngoma ya Wongko. Watu kutoka nchi nyingine walikuja kucheza pamoja nao. Wageni hawa walipocheza, walifanya urafiki, na ulipofika wakati wa kurudi makwao, marafiki zao wapya waliwasindikiza sehemu fulani ya njia. Hii ilikuwa desturi yao.
Lakini kulikuwa na mwanamke mmoja aliyempenda rafiki yake kupita kiasi. Siku moja wageni walipokuja kucheza mjini, walipoondoka, kila mtu alikwenda kuwasindikiza marafiki zake njiani. Mbwa mmoja akaenda pamoja nao njiani. Walipokwenda umbali kidogo, baadhi ya vijana wakawaambia marafiki zao, "Kwaherini. Tutaonana tena mwezi ujao."
Baadhi ya wanawake wakarudi, lakini wengine wakawaambia marafiki zao, "Popote mtakapokwenda katika ulimwengu huu, tutakwenda. Mkifa, tutakufa pamoja nanyi."
Walipokuwa wamesafiri mbali, wakafika kwenye bonde kubwa. Kisha wanaume wote wakawaambia marafiki zao walioapa kufa pamoja nao, "Lazima mrudi sasa. Mwezi ujao ukiwa mpevu, tutakuja tena."
Kwa hiyo wote wakarudi, wote isipokuwa mmoja. Alisema lazima afuate hadi afike mahali alipoishi rafiki yake. Mbwa akabaki pamoja na mwanamke.
Mwanamume akamwambia mwanamke, "Rudi!"
Mwanamke akasema, "Hapana!"
Mwanamume akasema, "Ninakujali mno. Kaa mjini. Nikirudi, nitakuja kwako, lakini usinifuate tunakokwenda."
Mwanamke akasema, "Nitakwenda!"
Kile ambacho mwanamke huyu hakujua ni kwamba mwanamume huyu alikuwa mfu! Kulipokuwa na ngoma mjini, wafu walitoka makaburini mwao na kucheza pamoja na walio hai, lakini watu hawakugundua upesi kwamba walikuwa wakicheza na wafu. Walipogundua, waliwaambia wanawake wote, "Watu wanapokuja kutoka nchi za mbali kucheza, msiende pamoja nao. Wakati mwingine wanaweza kuwa wafu, nanyi hamtajua."
Msichana huyu pia alikuwa ameonywa: "Wafu hutoka kaburini kucheza ngoma, kwa hiyo usifanye urafiki na wale wanaotoka mbali." Lakini mwanamke alikuwa mkaidi, na alikuwa amemchukua mfu huyu kuwa rafiki yake.
Walipokwenda mbali kiasi kwamba wafu wengine walikuwa wametoweka kurudi makaburini mwao, alibaki mwanamume mmoja tu. Yeye na msichana huyu wakaenda mjini kwake, lakini mwanamke hakujua kwamba huu ulikuwa mji wa wafu. Walipofika, walifika usiku na wakakuta nyumba moja tu mahali pale.
Msichana akaona mahali pale pote ni peupe, hakuna kitu ila wafu waliovaa nguo nyeupe. Mwanamume alikuwa ametoweka kando yake, na mwanamke huyu alikuwa ndani ya nyumba peke yake. Wafu walikuja kumlaani na kumsonya, si zaidi ya hapo, lakini mwanamke aliogopa vibaya mno. Hakuwa na mtu yeyote. Aliona nguo nyeupe tu; walimsonya na kutoweka tena. Aliweza kuwasikia lakini hakuweza kumwona mtu yeyote.
Lakini je, ulijua kwamba mbwa wana nguvu za ajabu? Mbwa aliweza kuwaona wafu, na akaanza kuwabwekea ili warudi. Kisha mbwa huyu akajigeuza kuwa mtu na akamuuliza mwanamke, "Nikikuokoa kutoka katika shida hii na kukurudisha nyumbani, utakapowapikia marafiki zako nami nikaiba wali na samaki wote, ukiniita 'mbwa,' utakufa." Hakutaka msichana amwite mbwa kwa sababu alikuwa amekuwa mtu.
Msichana akakubali na kusema, "Njoo, unirudishe." Mbwa akajigeuza tena kuwa mbwa ili aweze kuwabwekea wafu. Akasimama mbele, na wafu walipokuja, akawabwekea, nao wakarudi nyuma.
Msichana na mbwa walipokwenda mbali njiani, hawakuijua nchi na wakafika kwenye mto mkubwa. Hawakujua jinsi ya kuuvuka. Mbwa akasema, "Njoo, lala mgongoni mwangu." Kwa hiyo msichana akalala, na mbwa akambeba kuvuka maji makubwa. Walipokwisha kuvuka, mwanamke akamshukuru mbwa sana.
Mbwa akasema, "Napokea shukrani zako, lakini hupaswi kuniita 'mbwa' utakapofika mjini. Lazima unipe jina lingine zuri kama la mtu." Hakutaka kubaki mbwa watakapofika mjini kwa sababu watu wangemuuliza msichana, "Mbwa aliyekufuata yuko wapi?"
Mbwa akambeba mwanamke hadi walipofika nyumbani. Mwanamke akawaeleza watu wake taabu zote alizoziona. Akasema, "Kitu hiki kilichotufuata kimeniokoa," lakini hakumwita 'mbwa.'
Watu wa msichana wakamtendea mbwa huyu vizuri. Haikujalisha kama watu wengine walimwita mbwa, lakini msichana peke yake hakupaswa kumwita mbwa. Siku moja mwanamke akawapikia marafiki zake wali mzuri, mtamu, si kwa wafu, bali kwa marafiki wengine mjini. Alipomaliza kuupika na kwenda kuwaita marafiki zake waje kula wali, aliporudi, akakuta umeliwa. Hakusema lolote; akapika wali zaidi na kuwapa marafiki zake. Mbwa aliendelea kula wali aliopika msichana kila mara.
Siku moja akamkasirikia mbwa. Alikuwa amepika wali mzuri na nyama ya ng'ombe yenye mafuta kwa ajili ya marafiki zake wema mjini. Alipokwenda kuwaita marafiki zake, akakuta mbwa amekula wali mtamu na amelala karibu na bakuli tupu. Mwanamke akakasirika mno na kusema, "Mbwa huyu anaiba wali wangu kila mara! Tazama jinsi alivyoiba wali niliowapikia marafiki zangu!" Msichana alipomwita 'mbwa,' mbwa akamtazama, na msichana akaanguka akafa.
